Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida
(Hospitali ya Mkoa)

Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida yazinduliwa rasmi.

Posted on: December 20th, 2019

Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida imezinduliwa rasmi leo tarehe 20 Septemba, 2019 na Mhe. Mhandisi Jackson Masaka mkuu wa wilaya ya Mkalama kwa niaba ya Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi.

Wajumbe walioteuliwa ni, Mhe. Fatuma Hamisi Massengi (M/kiti wa Bodi) Dkt. Anuary Milulu, Bw. Innocent Arbogost, Bw. Liana Hassan, Pr. Bernard T. Ngalya, Bw. Kitila Mkumbo, Bi. Grace Kishindo, Bw. Ivo Manyaku, Mhe. Diana Chilolo, Bw. Athumani S. Bunto, Dkt. Victorina Ludovick, Dkt. Aubrey Mushi na Dkt. Deogratias Banuba (Mganga mfawidhi na katibu wa Bodi).

Katika hotuba yake mgeni rasmi Mhe. Mhandisi Jackson Masaka, mkuu wa walaya ya Mkalama kwanza kabisa amemshukuru Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi mkuu wa  mkoa wa Singida kwa kumpa nafasi ya  kukutana na watu wakubwa na muhimu sana, akiwataja baadhi ya wajumbe wa bodi na kuelezea furaha yake juu ya umakini uliotumika katika uteuzi wa wajumbe wa bodi hii ya ushauri.

“Na nimefurahi kuona wajumbe wa bodi ni watu ambao wameteuliwa kwa makini sana, hongereni sana. Kwa hiyo naamini tupo timu ambayo imekamilika vizuri sana, lakini kizuri zaidi naona tuko “Gender balanced” tuna mchanganyiko wa akina baba na akina mama, kwa hiyo tunapopanga, tunapanga maswala ambayo yanahusu jamii kamili”. Amesema Mhe. Mhandisi J. Masaka.

Mh. Masaka amesema kuwa amepata taarifa kuwa Hospitali hii imekua ikiendeshwa bila kuwa na bodi ya ushauri kwa muda wa miaka mitatu, imekuwa ikiendeshwa na mganga mfawidhi pamoja na timu yake ya menejimenti chini ya usimamizi wa katibu tawala wa mkoa. Pia amepata taarifa kuwa bodi hii iliyoundwa ni bodi ya ushauri ambayo itahakikisha kuwa kazi zinazofanyika zinafanyika vizuri ambazo lengo lake ni kuboresha utoaji wa huduma za afya.

Pia amewaeleza wajumbe wa bodi kuwa inapoundwa bodi tunaamini kabisa wajumbe wa bodi watakuwa mstari wa mbele, watakuwa waaminifu, watakuwa makini kuhakikisha kwamba bodi yetu inafanya kazi vizuri na hospitali yetu inaendelea vizuri. Amewaeleza wajumbe kuwa wao ndio wanaotakiwa kuisemea hospitali katika masuala ya tiba, maendeleo, mafanikio na palipo na mapungufu wao waisemee na hata ikitokea shida kwa watumishi wao wanapaswa kuwa wa kwanza kujua kuna shida gani na waweze kusema vizuri.

Mhe. Mhandisi Masaka amewaambia wajumbe wa bodi kuwa wao ndio wasimamizi wa sera inayohusika na tiba na uendeshaji wa Hospitali na ameeleze mambo mawili ambayo yanatofautisha bodi na menejimenti kuwa, kwanza bodi inahusika na sera za nchi katika maswala ya tiba, wao ndio wasimamizi na menejimenti wanatakiwa kuweka mikakati ya utekelezaji wa sera. Pili menejimenti wakishaweka mikakati ya utekelezaji wa sera wataileta kwenye bodi kwaajili ya kuridhiwa na ikisharidhiwa na bodi wanaitekeleza.

Pia amewaeleza wajumbe kuwa wanaanzia mahali pazuri kwakuwa hospitali sasa imepata mafanikio makubwa katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano lakini watakuwa na changamoto ya kuongeza mafanikio na kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana hayapungui ikiwa ni pamoja na mafanikio ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa asilimia 99 lakini amewataka kukabiliana na changamoto ya kupunguza idadi ya vifo vinavyoweza kuzuilika au vinavyotokana na sababu za kiutendaji na vibaki na vifo ambavyo ni vya asili yaani mtu amezeeka au amepata ajali mbaya isiyotibika.

Mgeni rasmi amewasisitiza wajumbe wa bodi kufanya kazi kwa uadilifu, kwa uaminifu na wafanye kazi kwa kuipenda Tanzania, kwa kuipenda Singida na kuwapenda watu wanaopata huduma katika hospitali hii ya rufaa ya mkoa wa Singida.

Akiendelea na hotuba yake amewataka wajumbe wa bodi kuangalia msimamo wa serikali, matakwa ya Mhe. Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania na maelekezo ya waziri wa afya, wayachukue na kuona kama yanatekelezwa. Amewataka wajumbe wa bodi kuhakikisha wanaondoa ule matazamo wa wananchi kuwa taasisi za serikali huwa hazifanyi vizuri ikilinganishwa na taasisi binafsi na ifikie mahali hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida ifanye vizuri sawa na hospitali binafsi na kuzidi.

Wajumbe wametakiwa kuuelewa mfumo wa utendaji wa tiba na kujua pale linapotokea tatizo wamuwajibishe nani, pia kuisimamia mifumo hiyo, kuweka mifumo ya kupima utendaji na utoaji wa motisha kwa watumishi ili kufikia lengo la kutoa huduma bora za afya.

Pia amemueleza mganga mfawidhi pamoja na timu ya uendeshaji wa hospitali kuwa sasa wasiendeshe hospitali kama vile haina bodi. Mgeni rasmi amesema;

“Sasa niseme na watendaji na kwa kuwa mganga mfawidhi upo, usiende kama vile hakuna bodi, sasa bodi ipo, msiendeshe hospitali kama vile hakuna bodi, hii bodi ni ya wananchi, hii bodi ni ya serikali”.

Awali akitoa taarifa ya hospitali, mganga mfawidhi Dkt. Deogratias Banuba (Daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa) amesema kuwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida ilianzishwa mwaka 1954 ikitumika kama hospitali ya wilaya, ilipandishwa daraja kuwa hospitali ya mkoa mwaka 1963 wakati huo ikihudumia kiasi cha wakazi 336,204, kwa sasa idadi ya wakazi imeongezeka na inakadiriwa kuwa 1,551,000. Hospitali inahudumia kati ya wagonjwa300-600 kwa siku ikiwa na viatanda 275, wodi 15 na inalaza wagonjwa kati ya 93-150 kwa siku.

Dkt. Banuba ameeleza kuwa mahitaji ya huduma bora yameongezeka, wagonjwa nao wanaongezeka, magonjwa nayo yameongezeka na uhitaji wa mafunzo kwa watumimishi umeongezeka. Aidha hayo yakijumuishwa na ongezeko la maradhi na ajali za barabarani lilizaliwa wazo la kuanzishwa ujenzi wa hospitali mpya itakayoweza kukabiliana na changamoto hizo.

Ameeleza kuwa hospitali ina eneo la hekta 126.5 ambapo hekta 1.5 ni eneo la hospitali ya zamani iliyopo kata ya Ipembe na hekta 125 ni eneo la mradi wa ujenzi wa Hospitali mpya iliyopo kata ya Mandewa. Pia hospitali ina jumla ya watumishi 346 sawa na asilimia 50 huku watumishi 13 wakiwa masomoni wakisomea fani mbali mbali zikiwemo za kibingwa na fani zingine.

Dkt. Banuba ameeleza kuwa hospitali imepata mafanikio makubwa katika kipindi hiki cha miaka minne ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa ni pamoja na; Kupatikana kwa huduma za kibingwa, kupatikana kwa vifaa tiba na vitendanishi ikiwemo X-ray na Ultrasound, Kuongezeka kwa mapato ya hospitali kulikotokana na serikali kuweka matumizi ya mifumo ya makusanyo katika hospitali za rufaa za mikoa nchini na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato, Kupungua kwa idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa kutoka 40 na kufikia 17 kwa mwezi Novemba, Kupungua kwa idadi ya vifo, Kuongezeka kwa wigo wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kufikia karibu asilimia mia moja na kupungua kwa gharama za misamaha na pia hospitali imefanikiwa kuwapeleka madaktari wanne kusomea masomo ya ubingwa katika fani za uzazi na magonjwa ya kina mama, magonjwa ya ndani, Dharura na udaktari bingwa wa watoto na hospitali inawalipia gharama za masomo.

Pia Dkt. Banuba ametaja changamoto zinazoikabili hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida kuwa ni pamoja na Upungufu wa watumishi. Ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) na kulazimika kuazima kwa majirani. Upungufu wa vifaa tiba. Kuchelewa kwa fedha za kuendeleza ujenzi wa hospitali mpya ya rufaa iliyopo kata ya Mandewa kwa wakati na kuchelewesha kuhamisha huduma zilizobaki hospitali ya zamani kwenda hospitali mpya na kupekekea changamoto ya uendeshaji wa hospitali mbili kwa mara moja. Changamoto ya maji chumvi ambapo kunahitajika mfumo wa kuvuna maji ya mvua kwaajili ya utakasaji wa vyombo vya chumba cha upasuaji na chumba cha uzazi. Kuchelewa kwa fedha za matumizi mengeneyo (OC) na kupelekea kutumia fedha za mapato ya ndani.

Katika uzinduzi wa bodi wajumbe walipatiwa mafunzo ya uendeshaji wa bodi yaliyotolewa na maofisa kutoka wizara ya afya na kupata fursa ya kuuliza maswali mbali mbali yaliyopatiwa majibu.

Aidha wajumbe wa bodi walipata fursa ya kutembelea eneo la mradi wa ujenzi wa hospitali mpya iliyopo lata ya Mandewa na kuona jinsi inavyofanya kazi lakini pia wameona mahali ambapo ujenzi umekwama na mwenyekiti akawaeleza wajumbe wa bodi kuwa wakatafakari jinsi ya kufanya ili kuendeleza ujenzi huo na watakapokutana katika kikao chao cha kwanza wachange mawazo ya kutatua changamoto hiyo.


Mwenyekiti wa bodi Mhe. Futuma Hamisi Massengi (Jaji mstaafu) amewaeleza wajumbe wa bodi kuwa wafanye kazi kwa kushauriana, kupendana na kuwa wataheshimu mawazo yao na amemuhakikishia Mganga mfawidhi kuwa bodi aliyonayo anaamini kuwa itamsaidia. Pia ameomba kuwa vikao vya bodi vyote vinne kwa mwaka vifanyike na amesema kuwa hakuna mjumbe atakaeshindwa kuhudhuria kikao kwasababu hakupewa posho bali akitaka kuchangiwa wajumbe wanaweza kumchangia.

Aidha wajumbe wote wamemshukuru Mhe. Ummy Mwalimu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto kwa kuwaamini na kuwapa nafasi ya kuwatumikia watanzania.