Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida
(Hospitali ya Mkoa)

MGANGA MFAWIDHI AWATAKA WATUMISHI KUSIMAMIA MAPATO

Posted on: March 5th, 2021

Akizungumza katika kikao cha watumishi wote kilichofanyika katika ukumbi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Singida, Kaimu mganga Mfawidhi Dkt. Ramadhani Kabala amewataka watumishi wote kusimamia makusanyo ya Hospitali. Aliwaeleza watumishi kuwa huduma zote za matibabu pamoja na shughuli zingine za Hospitali zinategemea sana makusanyo ya ndani ya hospitali.

“Kutokukusanya hatumkomoi mtu yeyote bali sisi wenyewe, tusipokusanya tutaishia kukosa dawa, vitendanishi na vifaa tiba na yawezekena sisi ndio tukawa wagonjwa na kuhitaji huduma.”

Hivyo kila mtumishi katika sehemu yake ya kutolea huduma ahakikishe huduma zote zinazopaswa kulipiwa zinalipiwa na kuhakikisha kuwa tunazuia upotevu wa mapato ya bima kwa kutoa huduma kwa usahihi ili kuondoa kabisa makato yatokanayo na makosa mbali mbali. Pia kuhakikisha fomu zote na nyaraka za matibabu ya wagonjwa wanaolipiwa gharama na mfuko wa bima zinatunzwa vizuri na kuwasilishwa mapema kwaajili ya malipo.

Dkt. Kabala alieleza kuwa kusimamia mapato na kuongeza mapato kuende sambamba na utunzaji wa vifaa na vitendea kazi tunavyotumia katika sehemu zetu za kutolea huduma.

Katika kikao hicho ilitolewa tahadhari ya magonjwa ya kuambukiza. Tahadhari hiyo ilitolewa na muuguzi mfawidhi Bi. Theresia P. Ntui. Alieleza kuwa kila mtumishi achukue tahadhari kila amhudumiapo mgonjwa kwa kuhakikisha kuwa anavaa Barakoa, kuvaa mavazi ya kujikinga (PPE), kunawa mikono mara kwa mara. Pia Bi. Theresi alishauri kupunguza idadi ya ndugu wanaokuja kusalimia wagonjwa.

Kuhusiana na magonjwa ya kuambukiza Dkt. Ramadhani Kabala alisema kuwa dunia kwa sasa imekumbwa na janga la “COVID 19” hivyo kila mtu achukue tahadhari kadiri anavyoweza kuhakikisha hapati maambukizi ya ugonjwa huu. Alisema asilimia kubwa ya wagonjwa wanapona lakini isiwe sababu ya mtu yeyote kutochukua tahadhari kwani hatujui athari za ugonjwa huu baada ya miaka kumi au zaidi ijayo kwa wale watakaokuwa wamepona.

Dkt. Kabala alitolea mfano magonjwa yaliyosumbua miaka ya 1970 ukiwemo ugonjwa wa Gonorhea. Alisema wengi wa wagonjwa walipona wakati huo wakiwa vijana lakini sasa wanarudi hospitali wakiwa ni wazee wakisumbuliwa na magonjwa ya mfumo wa mkojo. Kwa kuwa “COVID 19” inahusisha mapafu tuchukue kila tahadhari ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza baada ya muda kupita.

Kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza ya Presha, Kisukari na uzito uliopitiliza, Dkt. Kabala alisema kuwa magonjwa hayo yanatokana na mtindo mbaya wa maisha. Alisema watu wanapaswa kubadilisha mtindo wao wa maisha na kufanya mazoezi mara kwa mara kwani magonjwa yasiyo ya kuambukiza husababisha kinga za mwili kuwa chini na mtu huwa katika hatari kubwa ya kupata magonjwa yakuambukiza.

Aidha Bi. Mary Mwacha ambaye ni afisa utumishi alitoa ufafanuzi wa mambo kadhaa ya kiutumishi. Aliwataka watumishi wa kada zote kuzingatia miiko ya taaluma zao na kuwahudumia wagonjwa kwa upendo na kuwa na kauli nzuri kwa wagonjwa. Alieleza kuwa utoro ni kosa la kikanuni katika kanuni za utumishi wa umma na kwamba mtumishi yeyote hapaswi kutoroka.

Alisema; “Utoro ni kosa la kikanuni, siku 5 mfululizo utakua umejifukuzisha kazi, hairuhusiwi kutoroka hata siku moja kwani kwa sasa kanuni zinaruhusu kujumlishwa kwa siku ambazo mtumishi amekuwa mtoro na kufunguliwa mashauri ya kinidhamu.”

Bi. Mwacha amekemea rushwa kwa watumishi akisema kuwa rushwa ni adui wa haki hivyo ni marufuku kwa mtumishi kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa. Pia amesema ulevi uliopitiliza nao ni kosa la kinidhamu na hupelekea kuchafua taswira ya taasisi.

Bi. Mwacha amewataka watumishi wote kuwahi kazini kila wakati wa zamu zao na kuwahudumia watu wote kwa upendo na usawa. Akichangia suala hili kaimu mganga mfawidhi Dkt. Kabala amewataka watumishi wote wawe wanakaa katika maeneo yao ya kazi. Amesema kuwa hospitali imeweka utaratibu wa vibali kwa watumishi wanaotoka nje ya vituo vyao vya kazi, ameagiza kuwa vibali hivyo vitumike na asiwepo mtumishi atakayetoka nje ya kituo chake cha kazi bila kibali.