Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Atembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida
Posted on: March 8th, 2026Ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Ndugu Ismail Rumatila katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida imelenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la UVIKO-19 lenye gorofa tatu linalojengwa kwa fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika ziara hiyo, Ndg. Rumatila amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unafanyika kwa viwango bora vinavyotakiwa na kukamilika kwa wakati, huku akibainisha kuwa Serikali inaendelea kutafuta rasilimali zaidi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Mbali na kukagua mradi huo, pia alitembelea wodi ya wazazi na wodi ya akina mama waliojifungua kwa upasuaji, akijionea huduma zinazotolewa hospitalini hapo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Victorina Ludovick, amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kwa sasa ina madaktari bingwa 23, na hivi karibuni hospitali hiyo itaanza kutoa huduma ya Dialysis, hatua itakayosaidia kupunguza adha ya wagonjwa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo. Pia ameeleza kuwa watumishi 520 wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida walipatiwa mafunzo ya huduma bora kwa mteja ili kuimarisha ubora wa huduma kwa wananchi.

Nae Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Dkt. Muhaj Kamtande, amesema hospitali inaendelea kupanua wigo wa huduma za kibingwa na kwa sasa huduma za kibingwa zinazotolewa hospitalini hapo ni pamoja na huduma za kibingwa za magonjwa ya kina mama na uzazi, watoto, magonjwa ya ndani, ngozi, macho, meno, sikio pua na koo (ENT), upasuaji, upasuaji wa mifupa pamoja na huduma za kibingwa za radiolojia, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya hospitali kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Singida na maeneo jirani.



