Dkt. Banuba amehimiza ukusanyaji wa mapato ukiendana na ubora wa huduma
Posted on: December 15th, 2019Mganga mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida Dkt. Deogratias Banuba (Daktari bingwa wa upasuaji mifupa) amehimiza kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Hospitali ukiendana na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wagonjwa. Ameyasema hayo katika kikao cha watumishi kilichofanyika hospitalini hapo jana tar 18/12/2019.
Akizungumza wakati akiwapongeza idara ya upasuji kwa kuwa wa kwanza katika “5s KAIZEN na ISS” (mganga mfawidhi amewataka wakuu wa idara pamoja na wakuu wa vitengo na sehemu kuhakikisha wanafanya vizuri katika ubora wa huduma na kukusanya mapato.
5s ni dhana ya ubora wa huduma kwa kutumia S 5 ambazo ni Sasambua, Seti, Safisha, Sanikisha na Shikilia (Set, Sort, Shine, Standardize and Sustain) halafu ISS (Internal Supportive Supervision) ni Usimamizi shirikishi wa ndani.
Kikao hicho kiliambatana na utowaji wa zawadi kwa idara zilizofanya vizuri katika “5s KAIZEN na ISS” kwa robo ya kwanza ya Julai- Septemba 2019, ambapo idara ya upasuaji ilishika nafasi ya kwanza na kupata Cheti, Kikombe na fedha taslimu sh. 400,000 ikifiatiwa na idara ya maabara ambao walipata cheti na fedha taslimu Sh. 200,000 na ya tatu ikiwa ni idara uzazi na magonjwa ya kinamama waliopata cheti na fedha taslimu sh 100,000.
“Tunayafanya haya lengo likiwa ni kutoa motisha, tunajua hela haitoshi haijawahi kutosha hata siku moja, lakini tunataka kuonyesha kwamba tunafahamu na kutambua kazi ambazo mnazifanya katika vitengo vyenu, kwamba tunawakubali, mnafanya vitu vikubwa.” Amesema Dkt. Banuba.
“Kuna mtu labda ambaye sio kwamba moja kwa moja unaweza kukusanya mapato, hapana lakini unaweza ukajitafakari kwamba, hivi mimi hapa nilipo nimeboresha nini hapa kwenye hospitali au nipo kama mzigo tu.” Amesema Dkt. Banuba.
Dkt. Banuba amewataka wakuu wa idara na vitengo kuangalia ni sehemu gani ambayo inawapunguzia maksi ili waifanyie kazi. Wanapokaa katika idara zao waangalie kama wanatosha na wanaingiza nini? Amewataka wajue wanachokiingiza hospitali kwa kila siku na kujisikia vizuri na sio mtu akiulizwa ameingiza shilingi ngapi anakua hajui yeye anajua wagonjwa waliotoroka tu.
Aidha akizungumza katika kikao hicho Dkt. Banuba amepiga marufuku watumishi kusafiri bila kuwa na fomu zao za ruhusa. Akizungumzia ajenda ya maadili na uwajibikazi kwa watumishi, amesema;
“Nikianza kwa mfano na ruhusa, faili linakuja ofisini mtu ameshaondoka, sasa mimi niwaambie tu hauruhusiwi kuondoka bila kuwa na ruhusa yako mkononi, huko uliko hata kama utakuwa umefika Bukoba utarudi.”
“Unaomba ruhusa siku ya ijumaa jioni na uanatakiwa kusafiri Jumatatu sasa wewe hiyo ruhusa yako utaipata vipi? Hapo tutalaumiana” Aliongeza Dkt. Banuba.
Muuguzi mfawidi Bibi Theresia Ntui pamoja na Katibu wa hospitali Bw. Patrick Mosha wamawataka watumishi kuvaa mavazi yanayoruhusiwa wawapo kazini. Bibi Theresia amewataka wauguzi kuvaa mavazi yao kulingana na muongozo wa baraza la wauguzi na wakunga na Bw. Patrick alikataza uvaaji wa suruali za jinsi, uvaaji wa suruali chini ya kiuno na uvaaji tisheti kwa siku za kazi.
Akizungumzia uwajibikaji Muuguzi mfawidhi alisema “Sisi watumishi wa umma tunapaswa muda wote uwapo zamu tupatikane maeneo yetu ya kazi na tuwajibike katika kutekeleza majukumu yetu na katika kutekeleza hayo majukumu nasisitiza utunzaji wa kumbu kumbu (Documentation) kila tunachokifanya tuhakikishe tunakirekodi kwasababu hizo nyaraka zinaweza kutusaidia sisi kwa namna moja au nyingine. Wagonjwa wanaweza kulalamika ila kama umeweka vizuri taarifa zako zinaweza zikakutetea”.
Aidha amesisitiza utunzaji wa mali ya serikali akisema kuwa “Mali ya serikali ni wajibu wetu kuitunza na kuhakikisha inakuwa salama wakati wote, kwa hiyo kama tutaona kuna mtu anahujumu au anatendea ndivyo sivyo mali ya serikali tunapaswa kuingilia kati na kutolea taarifa.”
Pia muuguzi mfawidhi amewataka wauguzi kuwa wanapatikana kila mara wanapohitajika (Flexibility) ili kukava pengo la upungufu wa watumishi ili huduma zisisimame. Waepukane na ulevi kwani mtu akilewa hatakumbuka kuja kazini. Amewataka watumishi kutambua kuwa wao ni taswira ya hospitali na hivyo wanapaswa kujiepusha na ulevi wa pombe, madeni yaliyokithiri na kuwa waaminifu na kuacha kuchukua rushwa au fedha kwa wagonjwa.
Aidha Mganga mfawidhi amesema amekua akipata changamoto ya kufanya kesi za madeni ya watumishi ofisini kwake na sasa amesema hatashughulika na kesi yeyote ya madeni yasiyo rasmi. Amewataka watumishi kuepuka kukopa katika taasisi ambazo hazijasajiliwa au watu binafsi wanaokopesha kwa riba.
Aidha Dkt. Banuba amefungua milango kwa mtumishi mwenye dharura kuja kwake na kukopa fedha pasipo riba na kuweka utaratibu wa kurejesha fedha hiyo. “Sasa usije wewe kukopa wakati unajua katika sehemu yako wewe huingizi mapato. Moja wapo ya kazi ya taasisi ni kusaidia watumishi wake ikiwa ni pamoja na kuepuka mikopo ya riba kwenye makampuni yasiyo na tija kwa watumishi na kupelekea kushtakiwa mahakamani” Amesema Dkt. Banuba.