Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida
(Hospitali ya Mkoa)

MH. DR. TULIA AKABIDHI GARI LA WAGONJWA NA VIFAA TIBA

Posted on: September 26th, 2019

Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Dr. Tulia A. Mwansasu (Mb) akabidhi gari la wagonjwa pamoja na vitanda katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika viunga vya hospitali ya rufaa ya mkoa Singida.

Mh. Dr. Tulia amekabidhi  gari hilo lenye thamani ya shilingi milioni 21 pamoja na vitanda 16 vya wagonjwa ambapo viwili kati ya hivyo ni vitanda vya kujifungulia kina mama.

Gari hilo pamoja na vitanda vimetolewa na mbunge wa viti maalum mkoa wa Singida Mh. Aysharose Mattembe ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi makini wa Mh. Dr. John P. Magufuli katika kuboresha huduma za afya nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika tarehe 15 Septemba 2019, Dr. Tulia alisema, 

"Nikiwa kama kiongozi wa wabunge nawafahamu wabunge wote na kazi za maendeleo wanazozifanya katika majimbo yao hivyo ni seme kiukweli Aisharose Matembe anafanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wa mkoa wa Singida tena anatoa na fedha zake binafsi hivyo anapaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo wa mkoa wenu"  

Aidha Dr. Tulia amesema Mbunge Mh. Aisharose Mattembe anatekeza kwa moyo ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) ameyasema hayo katika hafla hiyo ambayo imehudhuriwa na mkuu wa mkoa wa Singida Mh. Dr. Rehema Nchimbi, viongozi waandamizi wa mkoa, Uongozi wa hospitali, watumishi na wanannchi mbali mbali.

Akizungumza katika hafla hiyo Mh. Aisharose Mattembe (Mb) amesema kuwa amekua akiumizwa sana na changamoto zinazowakabili wananchi ambazo amekua akikutana nazo kila anapokuwa katika ziara zake za kikazi kuwatembelea wananchi hasa changamoto zilizopo katika sekta ya afya zikiwemo mazingira bora ya kujifungulia kina mama na vitanda vya kulalia wagonjwa. Kama mbunge na kiongozi amekuwa akifanya ziara katika maeneo mbali mbali na kukutana na changamoto hizo.


Mh. Aisharose  amesema,

"Nimekuwa nikifanya ziara za kikazi mkoa mzima na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za wananchi kwa msaada wa serikali na wakati mwingine kwa kutumia fedha zangu".

Akizungumzia mgao wa msaada huo, Mh. Aisharose amesema, gari la kubebea wagonjwa pamoja na vitanda viwili vitabaki hospitali ya rufaa ya mkoa, vitanda viwili vya kujifungulia kina mama vitapelekwa zahanati za Tumuli iliyopo wilaya ya Mkalama na zahanati ya Mughanga inayohudumia vijiji vitano.  Zahanati zingine ni Ighombwe, na Kinyeto zilizopata  kitanda kimoja kila moja, zahanati ya Rungwa vitanda vitatu na vitanda vitano kwa kituo cha afya Sokoine.