Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida
(Hospitali ya Mkoa Mandewa)

MASHINE YA ZAIDI YA MILIONI 300 YA HUDUMA ZA PUA, KOO NA MASIKIO YAKABIDHIWA SINGIDA RRH

Posted on: March 19th, 2025

Kaimu katibu tawala Mkoa wa Singida ambae pia Ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick akipokea mashine ya kisasa ya uchunguzi na upimaji wa magonjwa ya Pua, Koo na Masikio machi 19 2025, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufanya maboresho ya huduma za kibingwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa.

 


 Amemshukuru pia Mdau D4D foundation kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kuwezesha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kupata mashine hiyo.



Nae Muwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Tiba kitengo Cha Usimamizi wa Tiba Hospitali za Binafsi na Umma (ADPPHS) Bi. Hilda Mushi kutoka Wizara ya Afya amefikisha Salam kutoka Wizara ya Afya akisisitiza juu ya huduma bora kuendelea kuzingatiwa katika utoaji wa huduma za Afya kwani Wizara ya Afya inaendelea kuboresha ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuiboresha sekta ya Afya.


Amesisitiza juu ya utunzaji wa mashine hiyo na kutumika kwa uangalizi ili iweze kudumu muda mrefu.


Akikabidhi mashine hiyo ya ENT Treatment Unit Mkurugenzi wa Shirika la D4D foundation Dkt. Denis Katundu ameishukuru Sekta ya Afya kwa ushirikiano wanaoendelea kuonesha katika kuboresha huduma za Afya “ mashine Hii inatoa huduma zaidi ya asilimia 80 za matibabu ya Pua, Koo na Masikio” .Dkt Denis Katundu

amewaahidi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida kuwa ushirikiano huu hautoishia hapo bali utaendelea. 


Kaimu Mganga Mfawidhi Wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida Dkt. David Mwasota ameishukuru Wizara ya Afya chini ya Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na mdau D4D foundation kwa kuwezesha kupatikana kwa mashine hiyo kwani itasaidia sana kupunguza Rufaa za kwenda kwenye Hospitali za kanda na hata Taifa, matibabu mengi yataishia Hospitalini hapo kutokana na ubora wa mashine hiyo.