Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida
(Hospitali ya Mkoa)

Mkuu wa mkoa ahimiza utunzaji wa mazingira sherehe za uhuru

Posted on: December 7th, 2019

Mh. Dkt. Rehema Nchimbi, mkuu wa mkoa wa Singida, amewataka wananchi wa mkoa huu kukataa uharibifu wa mazingira na kuacha kukata miti hovyo kwa tamaa na visingizio ambavyo kama vile  havina mbadala. Aidha amewataka viongozi wote wa serikali pamoja na viongozi wa dini kusimamia suala hilo. Ameyasema hayo katika sherehe za maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru na miaka 57 ya Jamhuri iliyofanyika kimkoa kwa zoezi la upandaji wa miti na usafi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida leo tarehe 9 Disemba, 2019.

Shereha za Maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika na miaka 57 ya Jamhuri ambayo kitaifa imefanyikia mkoani Mwanza, Mkoa wa Singida pia umeadhimisha sherehe hiyo ambayo imeongozwa na Mh. Dkt. Rehema Nchimbi ambaye ni mkuu wa mkoa wa Singida.

Sherehe ya mwaka huu imepambwa na kauli mbiu isemayo “Uzalendo, Uwajibikaji, Ubunifu ndio msingi wa maendeleo ya Tanzania”. Ratiba ya maadhimisho hayo kimkoa ilizingatia ratiba ya maadhimisho kitaifa ambapo Mh. Mkuu wa mkoa alitaka kutoa fursa kwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla ya kufuatilia matangazo ya moja kwa moja ya maadhimisho ya kitaifa ili kumsikiliza Mh. Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni.

Mkoa wa Singida umeadhimisha miaka 58 ya uhuru na miaka 57 ya Jamhuri kwa zoezi la kupanda miti na kufanya usafi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida. Katika maadhimisho hayo mh. Mkuu wa mkoa amesema;

“Kwa ishara hii ya kupanda miti tunajipa onyo sisi wana Singida na tunaweka ahadi sisi wana Singida kwamba Singida lazima iendelee kuwa njema, tena iendelee kuwa njema sana na Singida yetu hii lazima tukatae uharibifu wa mazingira. Tukieendelea kukatakata miti hii kwa tamaa na visingizio ambavyo kama vile havina mbadala hatutakuwa tunautendea haki uhuru wetu na hatutakuwa tunaitendea haki Jamhuri yetu”. Ameyasema hayo Mkuu wa mkoa Mh. Dkt Rehema Nchimbi.

Mkuu wa mkoa amesema kuwa wana wa Singida hatuna sababu ya kukata miti. Amesema, “Wale wanaokata miti kwa kisingizio cha wanatafuta fedha eti ndio ajira ya mkaa kwa maadhimisho haya ya miaka 58 ya uhuru na miaka 57 ya Jamhuri tukitakiwa kuwa wazalendo, wabunifu na wawajibikaji lazima tubadilike”

Mkuu wa mkoa amesema kuwa kiasi cha mkaa kinachotoka nje ya mkoa ni kikubwa mno, na kuwa watu wameacha miti ya barabarani  lakini ukiingia ndani miti imekatwa sana. Kwa maadhimisho haya amesema sasa ukataji wa miti basi. Mkuu wa mkoa amesema tunakauli mbiu yetu ya achia shoka shika mzinga. Tukifuga nyuki tutakua matajiri na tutakua na maisha bora kuliko kuchoma mkaa.

Aidha mkuu wa mkoa amesema kuwa Singida yetu ni njema na ndio maana tunatukuka na kwa kuwa mkoa ambao unatishia kwa kilimo cha korosho na sababu mojawapo ya kuingia kwenye “project” na programu ya kilimo cha korosho ni uhifadhi wa mazingira. Amesema mahali popote palipostawi korosho hali ya hewa huwa ni njema na uhifadhi wa mazingira huwa ni mkubwa. Sasa haiwezekani upande mmoja tuhamasishe kilimo cha korosho na tusifike, tufahamike kwa kilimo kikubwa cha korosho ambacho hakipo hapa nchini halafu upande mwingine watu wakate miti wachome mkaa.

“Kati ya club amabazo ningependa zianzishwe ni club za katazo la kuchoma mkaa kwa kauli mbiu yetu ACHIA SHOKA KAMATA MZINGA”. Amesema mkuu wa mkoa.

Amesema haiwezekani tukaendele kuwa huru iwapo msitu itakwisha, iwapo tutakuwa na ukame. “Sisi Singida hatuna ukame, tuna kilimo kinachotumia maji kwa ufanisi na ndio maana unaona Singida ni ya kijani na itaendelea kuwa ya kijani sana na hasa mikorosho inavyoendelea kustawi”. Ni maneno ya Mh. mkuu wa mkoa.

Mkuu wa mkoa amesema kuwa tunafahamu maana ya uhuru na sasa tuanze kuwa huru. Amesema tuna miaka 58 ya uhuru lakini tuna watu ambao bado hawapo huru, huwezi kuwa huru na ukawa na hasira mpaka ukamuua mke wako, ukawa na visasi vya kupitiliza mpaka mkauana hovyo hovyo. Halafu haiwezekani ukawa huru ukawa huwezi kuona fursa za maendeleo zilizopo katika mkoa Singida. Amewataka vijana kuwa huru na kulima zao la korosho na kuacha kukaa kwenye magenge na kupeana shuhuda zisizo na maana.

“Kuwa huru ni pamoja na kujitegemea, kuwa huru ni pamoja na kujithamini, kujipenda wewe mwenyewe, kuwa huru ni pamoja na kuona fursa kama nilivyosema za maendeleo yetu, kuwa huru ni pamoja na kuheshimiana”. Amesema mh. mkuu wa mkoa.

Mkuu wa mkoa ametoa rai na wito kwa kila mtendaji kuwa na sensa ya vijana katika eneo lake na ahakikishe kwamba vijana hao wana mashamba ya korosho.

Katika hatua nyingine mkuu wa mkoa ametoa zawadi Tsh. 187,450 kwa watoto 12 ambao wamezaliwa siku ya leo katika Hospitali ya rufaa ya mkoa na kituo cha afya Sokoine, zawadi iliyowasilishwa kwa walengwa na mganga mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Voctorina Ludovick.

Aidha Mwenyeji, mganga mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida Dkt.  Deogratias Banuba amemshukuru mh Mkuu wa mkoa kwa kuipa kipaumbele hospitali yetu na kuamua kufanyia sherehe za maadhimisho haya ya miaka 58 ya uhuru na miaka 57 ya Jamhuri katika hospitali yetu.

“kwa kweli tunamshukuru kwa kufanikisha zoezi hili kwa kuipa kipaumbele hospitali yetu angeweza kuamua hii shughuli kuifanyia sehemu nyingine aidha shuleni au mahali pengine lakini ameona ni muhimu kulifanyia hapa kwetu Hospitali”. Amesema  Dkt Banuba.

Aidha ameahidi kuitunza miti yote iliyopandwa katika zoezi la leo na kupanda miti mingine ya matunda na mkorosho kama alivyoagiza Mh. Mkuu wa Mkoa.