Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida
(Hospitali ya Mkoa)

MUUGUZI NA MSAIDIZI WA AFYA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SINGIDA WAPEWA MOTISHA KWA UTUMISHI ULIOTUKUKA

Posted on: January 26th, 2022

Motisha hizo zilitolewa baada ya kumalizika kwa robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2021/2022 mwezi huu wa kwanza. Wakiongea kwa nyakati tofauti Daktari kiongozi wa wodi ya kina mama waliojifungua kwa njia ya upasuaji Dkt. William Soa pamoja na Muuguzi kiongozi wa wodi hiyo Bi. Evelyne Kilimba walisema, kila baada ya miezi mitatu katika wodi yao huwa wana utaratibu wa kutoa motisha kwa watumishi waliothibitishwa kuwa na utumishi uliotukuka na huwa wana vigezo ambavyo wanaviangalia. Vigezo hivyo ni kama vile kuwahi kazini, utunzaji wa kumbukumbu, uvaaji wa unifomu, ujazaji wa opras, mahusiano kati ya mtumishi na watumishi wenzake pia na ubunifu katika kutekeleza majukumu yao.

Nae Katibu wa Timu ya Usimamizi wa Ubora wa Huduma Bi. Erica Charles aliwapongeza viongozi wa wodi hiyo kwa kusema utaratibu waliojiwekea wa kutoa motisha ya cheti na shilingi 50,000/= kwa aliyeshika nafasi ya kwanza na shilingi 25,000/= bila cheti kwa alieshika nafasi ya pili ni utaratibu mzuri ambao unapaswa kuigwa na wodi nyingine, idara nyingina pamoja na vitengo vingine. Katibu alisisitiza motisha hizo walizopata mshindi wa kwanza Bi. Neema Ndeiyaki Reuben ambae ni muuguzi na mshindi wa pili Mzee Salu Kija ambae ni msaidizi wa afya iwe ni chachu kwa watumishi wengine wa wodi ya kina mama waliojifungua kwa njia ya upasuaji.